Berlin. Bunge la Ujerumani laidhinisha katiba ya Ulaya, Chirac aipongeza ujerumani kwa hatua hiyo.
28 Mei 2005Ujerumani imeidhinisha katiba mpya ya umoja wa Ulaya, baada ya bunge kupiga kura ya kuikubali katiba hiyo.
Bunge la majimbo , Bundestag, limeidhinisha katiba hiyo wiki mbili zilizopita.
Ujerumani kwa hiyo ni nchi ya tisa kuweza kuidhinisha katiba ya umoja wa Ulaya.
Ili Katiba hiyo iweze kufanya kazi inatakiwa kuidhinishwa na mataifa yote 25 wanachama wa umoja wa Ulaya.
Rais wa Ufaransa Jacques Chirac katika barua yake ya kumpongeza kansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder amesema kuwa kuidhinishwa huko kwa katiba ya umoja wa Ulaya na Ujerumani, kunatoa ishara muhimu kwa wapiga kura wa Ufaransa. Hii inakuja siku moja baada ya Bwana Chirac kutoa wito kupitia televisheni kwa raia wa Ufaransa kuidhinisha katiba hiyo katika kura ya maoni itakayofanyika siku ya Jumapili.
Kura ya maoni iliyoendeshwa hivi karibuni inaonesha kuwa Wafaransa wanaweza kupiga kura kuikataa katiba hiyo.