BERLIN: Blair aikosoa Ujerumani.
9 Mei 2005Waziri mkuu wa Uingereza bwana Tony Blair amesema kwamba wajerumani wana haki ya kuzungumzia maafa yaliyowafika katika vita kuu ya pili ya dunia lakini wasijione kama wahanga wa vita hiyo.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Ujerumani, "BILD" waziri mkuu Blair pia amesema kwamba watu barani Ulaya wasikubali kujenga mawazo kwamba uhalifu dhidi ya binadamu hauwezi kutokea tena barani Ulaya.
Bwana Blair amesema anaelewa kwa nini baadhi ya wajerumani hawatathmini kusalimu amri kwa nchi yao katika vita kuu ya pili ya dunia kuwa tendo la kukombolewa lakini hatahivyo hayo hayamaanishi kwamba wajerumani sasa wajenge utamaduni wa masikitiko.
Wakati huo huo balozi wa Ujerumani nchini Uingereza bwana Thomas Matussek amesema kwamba kiherehere kinachofanywa na waingereza juu ya enzi za ufashisti katika Ujerumani na kukataa kuona mabadiliko ya kisasa yanayofanyika nchini humo, kinasababisha Ujerumani na Uingereza zifarakane.
Hatahivyo waziri mkuu Blair amehakikisha kwamba mahusiano baina ya nchi yake na Ujerumani ni mazuri.