Berlin: Bado unangojewa uamuzi wa kuwapeleka wanajeshi waq Kijerumani hadi Libanon.
3 Septemba 2006Uamuzi wa wa kuwaweka wanamaji wa jeshi la Ujerumani kufuatana na operesheni ya Umoja wa Mataifa katika Libanon umeahirishwa. Msemaji wa serekali, Ulrich Wilhelm, aliarifu kwamba kikao maalum cha baraza la mawaziri la Ujerumani kilichopangwa kufanywa kesho kuamua juu ya kutumwa wanajeshi hao kimevunjwa. Waziri mkuu wa Libanon, Fuad Siniora, amemuarifu Kansela Angela Merkel kwamba kutokana na mazungumzo yalioko ndani huko Libanon yeye hawezi kutoa ombi la jambo hilo kwa Umoja wa Mataifa. Bwana Wilhelm alisisitiza kwamba bila ya kutolewa ombi la Libanon kutaka wanamaji wa kimataifa, hakutakuweko suala la kuwatuma wanajeshi wa Kijerumani.
Wakati huo huo, kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametaka wanamaji wa Kijerumani wanaopangwa kuwekwa katika mwambao wa Libanon wawe na kibali cha kutumia nguvu. Alisema katika televisheni kwamba , kwa mfano, lazima waweze kuizuwia meli isiendelee kusafiri ili kuzuwia upelekaji haramu wa silaha. Kutokana na uamuzi unaotarajiwa kuchukuliwa na bunge la Ujerumani juu ya jambo hilo, mkuu wa wabunge wa Chama cha SPD, Peter Struck, alikubaliana na msimamo huo.