BERLIN : Angela Merkel kuwa Kansela wa Ujerumani
10 Oktoba 2005Kwa mujibu wa repoti ya kituo cha televisheni ya Ujerumani ZDF wakuu wa chama cha Christian Demokrat CDU na wale wa Social Demokrat SDP wamekubaliana kwamba Angela Merkel awe Kansela mpya wa Ujerumani.
Kituo hicho cha televisheni cha taifa hakikutaja duru za habari hizo na hakikutowa ufafanuzi zaidi.Uamuzi mwengine kuhusu baraza jipya la mawaziri ulioripotiwa na kituo hicho cha televisheni cha ZDF ni kwamba chama cha Social Demokrat kitapatiwa nyadhifa nane za uwaziri ambazo ni za wizara ya mambo ya nje,fedha,sheria,kazi, afya,uchukuzi,mazingira na maendeleo ya kimataifa.
Tangazo rasmi linatazamiwa kutolewa leo usiku baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa kwa maafisa waandamizi katika kila chama kwa ajili ya kuridhiwa.
Hatua ya Schroeder kuachia ngazi baada ya kuwa madarakani kwa miaka saba itamfanya Merkel kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Ukansela nchini Ujerumani.
Wote wawili Schroeder na Merkel walikuwa wakidai kwamba walikuwa wamejipatia mamlaka ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu ulioshindwa kutowa mshindi dhahiri hapo mwezi uliopita ambapo kwayo CDU ilikuwa ina wingi wa viti vinne zaidi bungeni kuliko SPD.