BEIRUT: Ujerumani imeahirisha kutuma jeshi la wanamaji
4 Septemba 2006Kikundi cha pili cha wanajeshi wa Italia kimewasili Lebanon,kusaidia tume ya Umoja wa Mataifa kulinda makubaliano ya kusitishwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah.Sasa Italia ina kama wanajeshi 3,200 kulinda amani nchini Lebanon.Umoja wa Mataifa unaitaka Israel iondoshe vikosi vyake vyote kutoka Lebanon,baada tu ya kuwasili kwa wanajeshi 5,000 wa kulinda amani.Ujerumani kwa hivi sasa imeahirisha kupeleka jeshi la wanamaji,kama sehemu ya tume ya Umoja wa Mataifa kulinda amani nchini Lebanon.Kansela Angela Merkel amesema,hawezi kuvituma vikosi hivyo siku ya Jumatatu kama ilivyotazamiwa kwa sababu bado haijapokea ombi rasmi kutoka Lebanon.Ujerumani imesema,ipo tayari kulinda pwani ya Lebanon ili kuzuia usafirishaji wa silaha kwa Hezbollah,lakini imekataa kupeleka vikosi vya ardhi kavu.