BEIJING : Sudan kutangaza mahkama kuwashtaki watuhumiwa wa uhalifu wa vita Dafur
21 Mei 2005Sudan ambayo imekataa kushtakiwa kwa raia wake kwenye mahkama ya kigeni inatazamiwa kutangaza kuundwa kwa baraza la mahkama kujaribu kuwashtaki watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa vita katika jimbo la Dafur hivi karibuni.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo mwezi wa Machi limetaka watuhumiwa wa uhalifu wa Dafur wafikishwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilioko The Hague nchini Uholanzi.Lakini pia limewacha mlango wazi kwa Sudan kuwahukumu watu hao katika mahkama zake yenyewe ili mradi zinakuwa za kuaminika kwa kusema kwamba Mahkama ya Jinai ya Kimataifa inapaswa kujashiisha juhudi kama hizo za ndani ya nchi.
Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Mustafa Osman Ismail ameuambia mkutano wa waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini China wanashirikiana kwa karibu na Umoja wa Afrika na kwamba anategemea kutangazwa hivi karibuni kwa mahkama hiyo,hakimu wake pamoja na mwanasheria mkuu.
Amesema kamati inayoongozwa na waziri wa sheria inatarajiwa kukamilisha mipango hiyo na kutangaza habari hizo kwa wananchi hivi karibuni.