BEIJING : China yafuta madeni ya zaidi ya dola bilioni 1 kwa Afrika
7 Julai 2005China taifa linaloinukia kuwa na nguvu kubwa za kiuchumi imesema leo hii imefuta madeni ya dola bilioni 1. 3 inazodai nchi za Kiafrika katika kipindi cha miaka miwili na imezitaka nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi za kimaskini kuondokana na umaskini.
Umaskini barani Afrika pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na bei ya mafuta ni masuala yaliyopewa kipau mbele kwenye agenda ya mkutano wa wiki hii wa viongozi wa kundi la mataifa manane yenye maendeleo ya viwanda duniani huko Scotland ambapo Rais Hu Jintao wa China anahudhuria kwa mara ya kwanza kabisa kwa ajili ya mazungumzo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba China inafuta madeni ya yuan bilioni 10 .5 inayodai mataifa 31 ya kimaskini na nchi zenye maendeleo duni za Kiafrika katika kipindi kisichozidi miaka miwili tokea ilipopitisha uamuzi huo hapo mwaka 2000.
Msemaji huo Lin Jintao ameukaribisha uamuzi wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa manane tajiri mwezi uliopita kufuta zaidi ya dola bilioni 40 za madeni ya nchi 18 za kimaskini kabisa duniani zikiwemo nchi 14 za Afrika.