BEIJING: China haina sababu ya kuiomba Japani msamaha
17 Aprili 2005China imeiambia Japani kuwa haina sababu ya kuomba msamaha,kufuatia mfululizo wa maandamano yaliofanywa dhidi ya Japani katika miji mbali mbali nchini China.Waziri wa mambo ya kigeni Li Zhaoxing amemuambia waziri mwenzake wa Japani,Nobutaka Machimura alie ziarani,kuwa serikali ya Japani kwa mfululizo imefanya mambo yalioumiza hisia za wananchi wa China.Machimura alikwenda China hii leo kulalamika kuhusu maandamano yanayofanywa dhidi ya Japani.Maandamano hayo yalichomoza baada ya serikali ya Tokyo kuidhinisha vitabu vya shule ambavyo waandamanaji wanasema vimepunguza uzito wa ukatili uliotendwa na Wajapani wakati wa vita vikuu vya pili nchini China.Wafanya maandamano katika miji mbali mbali ya China wanapinga pia juhudi za Japani kuwania kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.