Bayern Munich na Rwanda: Kwa nini udhamini unazua utata?
6 Februari 2025Mgogoro unaoendelea mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaonekana kuingia hadi katika sekta za michezo na utalii. Hii ni baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Dkt Thérèse Kayikwamba Wagner, kuitaka klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani kusitisha mkataba na Rwanda wa mwaka 2023, unaofuata nyayo za klabu ya Arsenal ya Uingereza na klabu ya Ufaransa ya Paris Saint-Germain.
Mkataba huo wa miaka mitano unaodhaniwa kuwa wa thamani ya zaidi ya dola milioni 5.15 kwa mwaka unaitaka Bayern kuitangaza kampeini ya kuvutia utalii ya Rwanda inayojulikana kama 'Visit Rwanda'.
Katika barua aliyoziandikia klabu tatu za Arsenal, PSG na Bayern, Kayikwamba amesema: Watu wengi wamepoteza maisha. Ubakaji, mauaji na wizi vimefanyika. Mfadhili wenu amehusika moja kwa moja na masaibu haya. Kama sio kwa dhamiri yenu kukatiza mkataba huu, basi kwa ajili ya waathiriwa wa uvamizi wa Rwanda.
Mabingwa hao wa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, hawajajibu swali la DW ama kuzungumzia hadharani suala hilo. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo mnamo mwaka 2023, Jan-Christian Dreesen, Mkurugenzi mkuu wa klabu hiyo ya Bayern, alitetea mkataba huo.
Soma pia: Bayern Munich yakosolewa dili lake la Visit Rwanda
Dreesen alisema kuwa ndio walichukuwa pesa kutoka Rwanda lakini pia wanafanya kitu kuzihusu, kama vile kuwa wazi kuzihusu, kutuma makocha Rwanda pamoja na kujenga chuo cha mafunzo kwa vijana.
Dreesen aliongeza kuwa wanataka kuwa sehemu ya maendeleo ya Rwanda na pia kuipiga debe Afrika kama bara lenye fursa.
Lakini je hii ndio mara ya kwanza kwa jambo kama hili kutokea kwa Bayern?
Jibu ni hapana. Kwa kweli mkataba wa Rwanda ulitiwa saini chini ya miezi miwili baada ya kumalizika kwa mkataba sawa na Qatar ambao pia ulionekana kuwa na utata mkubwa, na kusababisha mpasuko mkubwa kati ya klabu na mashabiki wake.
Msimamo wa Qatar kuhusu haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja, upinzani na masuala mengine ya haki za binadamu yaliangaziwa wakati wa Kombe la Dunia la 2022. Mashabiki sugu wa Bayern waliona kuwa siasa za nchi hiyo hazikuambatana na maadili mengi ya klabu hiyo na mkutano mkuu wa mwaka wa 2021 ulishuhudia machafuko katika matukio ambayo yaligonga vichwa vya habari duniani.
Soma pia: Kongo yakifungia kituo cha habari cha Al Jazeera
Lakini klabu hiyo ya Bayern pamoja na Rwanda zinanufaika vipi kutokana na mikataba kama hiyo?
Kwa upande wa klabu hiyo, jibu la kwanza linaonekana kuwa fedha, ingawa haiko wazi ikiwa kiwango husika ambacho kinaonekana kuweza kulipa tu mishahara ya nyota Harry Kane kwa miezi kadhaa ni muhimu ikilinganishwa na uharibifu wa sifa yake unaosababishwa na masuala kama hayo.
Bayern pia inatafuta kuboresha wasifu wake katika eneo hilo
Kwa Rwanda, lengo lililotajwa ni kusaidia maendeleo ya soka la vijana kwa wavulana na wasichana nchini humo kupitia shule ya mafunzo ya Bayern Munich iliyoanzishwa nchini humo. Haya ni kulingana na waziri wa michezo Aurore Mimosa Munyangaju.
Waziri huyo amesema kuwa uwezo upo kwa Wanyarwanda kufanya vyema katika soka na ushirikiano huo unatoa fursa kubwa kwa Rwanda kufanikiwa katika michezo.
Lakini waangalizi wengi wa kimataifa wana maoni tofauti, huku Rwanda, na kiongozi wake Paul Kagame,wakizidi kulaumiwa kwa kutumia michezo ili kutoa taswira ya umma ambayo haiakisi ukweli.
Hali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inasonga kwa kasi na haijulikani jinsi usitishaji mapigano ulivyo salama. Ufaransa imeitaka Rwanda inayodai kuwa Kongo kuondoka mara moja nchini humo, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, David Lammy, amesema M23 isingeweza kuchukua Goma bila msaada wa raslimali kutoka kwa vikosi vya ulinzi vya Rwanda nayo Ujerumani ni miongoni mwa mataifa makubwa yanayotafakari iwapo iendelea kutuma msaada Rwanda.
Kwa mtazamo wa Bayern, mambo hayako wazi. Kwa kuzingatia jinsi mashabiki wanavyojihusisha kisiasa nchini Ujerumani, ina uwezekano wa kujipata chini ya shinikizo la ndani zaidi kuliko PSG ama Arsenal, na kuhusiana na Qatar, lazima sasa iamue kama pesa ni muhimu zaidi ikilinganishwa na uharibifu wa sifa.