Kuwapokonya silaha Hezbollah ni suala la ndani la Lebanon
22 Julai 2025Matangazo
Mjumbe maalumu wa Marekani kwa ajili ya Syria Tom Barrack amesema kuwapokonya silaha wanamgambo wa Hezbollahni suala la ndani, huku serikali ya mjini Washington ikiendelea kuwashinikza viongozi wapya wa Lebanon walichukulie hatua kundi hilo lililodhoofishwa na vita na Israel.
Barrack ambaye pia ni balozi wa Marekani nchini Uturuki ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Beirut baada ya kukutana na waziri mkuu wa Lebanon Nawaf Salam kwamba litakuwa jambo la kuvunja moyo ikiwa Hezbollah hawatapokonywa silaha.
Awali hapo jana Barrack alikutana na rais wa Lebanon Joseph Aoun aliyemkabidhi rasimu ya muongozo wa utekelezaji wa ahadi za Lebanon tangu makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyoafikiwa Novemba mwaka uliopita.