Barcelona na PSG ndani ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa
16 Aprili 2025Haya yanafanyika wakati ambapo Real Madrid wana kibarua kigumu Jumatano dhidi ya Arsenal nao miamba wa Ujerumani Bayern Munich, wakiwa wana mlima wa kukwea dhidi ya Intermilan, Madrid na Bayern wote wakiwa walifungwa katika ungwe ya kwanza ya robo fainali.
Barcelona walisafiri Ujerumani kupambana na makamu bingwa wa Ulaya msimu uliopita Dortmund wakiwa kifua mbele 4-0 ila Dortmund waliwatia baridi kidogo kwani waliwafunga 3-1 katika uwanja wa Signal Iduna Park.
Serhou Guirassy alifunga mabao matatu ya Dortmund kwenye mechi hiyo waliyowalemea pakubwa hao wapinzani wao na Barca walipata la kufutia machiozi kupitia kwa Ramy Bensebaini aliyefunga kwa bahati mbaya katika lango lake.
Dortmund ilijilinda vyema
Kocha wa Dortmund Niko Kovac anasema amehuzunika kwa kuwa wameondolewa kwenye mashindano hayo ila ameridhika na anajivunia wachezaji wake kwa jinsi walivyocheza.
"Barcelona wamepoteza mechi kwa mara ya kwanza mwaka 2025. Hilo linasema kuhusiana na jinsi timu yangu ilivyocheza. Nawapongeza Barcelona lakini tumeridhika na matokeo," alisema Kovac.
Dortmund sasa watalazimika kugeukia ligi ya nyumbani Bundesliga ambapo wamekuwa na mchezo usioridhisha na wanaishikilia nafasi ya nane wakiwa kwenye hatari kubwa ya kutoshiriki mashindano hayo ya Ulaya msimu ujao.
Ama kwa Barcelona, kocha wao Hansi Flick amesema la muhimu kwao sasa ni kwamba wamefika nusu fainali ya ligi ya mabingwa licha ya kupoteza mechi ya jana.
"Tumecheza dhidi ya timu nzuri hapa Dortmund. Sitaki kusema mengi zaidi kuhusu timu yangu kwasababu haitokuwa sawa kwa Dortmund. Wamejilinda vizuri na wametupa wakati mgumu sana leo, ila tumetinga nusu fainali," alisema Flick.
Katika robo fainali nyengine jana kocha wa PSG Luis Enrique sasa anajitapa kwamba timu yake ndiyo yenye kikosi bora zaidi duniani. Enrique ameyasema haya baada ya kufuzu hiyo hatua ya nne bora licha ya kurambishwa mabao 3-2 na Aston Villa na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-4.
PSG sasa watakumbana na mshindi kati ya Arsenal na Real Madrid huku Barcelona wakiwa watapatana na mshindi kati ya Bayern Munich na Inter Milan ambao watacheza hii leo.
Arsenal na Inter wako kifua mbele katika mechi zao za usiku wa leo, Arsenal wakiwa waliwalima Real Madrid 3-0 huko London na Inter wakiwa walivuna ushindi wa 2-1 mjini Munich.
Hatuendi Madrid kujilinda
Kiungo wa Real Madrid Jude Bellingham amesema kauli mbiu iliyoko miongoni mwa wachezaji wa Madrid kuelekea mechi ya Jumatano ni kukipindua kipigo.
"Hakuna mengi unayoweza kuifanyia Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa ambayo hayajafanywa na leo ni fursa yetu kufanya kitu ambacho hakijafanywa kwa mara ya kwanza, na hilo ni muhimu sana kwetu," alisema Bellingham.
Kwa upande wa Arsenal wao nao wanaamini kwamba baada ya dakika tisini watakuwa washalisogeza guu la pili katika hatua ya nusu fainali. Huyu hapa mlinda lango wao David Raya.
"Chochote kinaweza kutokea katika kandanda. Tunakwenda kuicheza mechi hii tukisaka ushindi, hatuendi kujilinda tu, tutajituma kutoka dakika ya kwanza, tunataka kuishinda mechi hii, " alisema Raya.
Mechi zote mbili ya Madrid dhidi ya Arsenal na Inter dhidi ya Bayern zitachezwa kuanzia saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Vyanzo: Reuters/dpa