Baraza la waandishi habari Kenya lalaani matukio ya dhulma
6 Aprili 2021Baraza la waandishi wa habari nchini Kenya sasa linasema litahakikisha kila afisa wa polisi anawajibika binafsi kuhusiana na tuhuma za dhuluma dhidi ya waandishi wa habari. Hali ya uzembe kwenye idara ya polisi inalaumiwa kwa kuongezeka kwa visa vya waandishi wa habari kunyanyaswa mikononi mwa polisi.
David Omurunga mwandishi wa habari wa idhaa ya radio ya Milele FM nchini Kenya, hii leo amefika kwenye kituo cha polisi Nakuru mjini kuandikisha taarifa kuhusu namna maafisa wa polisi walivyomshambulia na kumdhihaki alipokuwa akitoka kazini mwendo wa saa mbili unusu wikendi hii.
Waandishi wa habari ni kati ya makundi ya wafanyikazi yanayoruhusiwa kuhudumu nje ya muda wa kubakia ndani
Wanahabari ni kati ya makundi ya wafanyikazi yanayoruhusiwa kuhudumu nje ya muda wa kutotoka nje uliowekwa na Rais Uhuru Kenyatta, alipotangaza sheria mpya za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona. Maafisa wa polisi hata hivyo, wamelaumiwa kutumia mamlaka waliyopewa kuidhinisha masharti haya, kuwahujumu wananchi. Kisa hiki kimeugadhabisha muungano wa kitaifa wa waandishi wa habari, mwenyekiti wa tawi la Nakuru Kioko Kivandi akiitaka taaluma hii kuheshimiwa.
"Waandishi wa habari ni kati ya watu wanaotoa huduma muhimu wakati huu taifa linapokabiliana na janga la COVID 19. Wanapaswa kuheshimiwa.”
Joseph Tonui, kamanda wa polisi kaunti ya Nakuru amezungumzia mapungufu katika njia za kutoa taarifa akisema wakati mwingi habari hizi haziwafikii.
"Hatutalikwepa suala hili, hawa ni maafisa wetu. Uchunguzi utafanyika na hatua itachukuliwa. Ni muhimu kufahamu kwamba jambo kama hili linapofanyika njia za kutoa malalamishi huwa ni nyingi.”
Baraza la kitaifa la wanahabari sasa linasema litaihusisha mamlaka huru inayowasimamia polisi, IPOA, kuhakikisha kuwa kila afisa wa polisi atakayetuhumiwa kumshambulia au kumdhulumu mwandishi wa habari anashtakiwa kibinafsi. Hii ni kutokana na hali ya kukwepa adhabu inayoendelezwa na idara ya polisi, kama anavyoeleza David Omwoyo, afisa mkuu wa baraza la kitaifa la wanahabari.
"Sio kwamba polisi hawajui wanavunja sheria, ni kwamba wanajua hawataadhibiwa. Na sasa tutaiandikia IPOA kwa sababu tunataka wakati kisa kama hiki kinatokea afisa wa polisi anafuatiliwa kibinafisi na kushtakiwa kivyake.”
Waandishi wa habari wanne wameshambuliwa na polisi katika kipindi cha mwezi mmoja na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
Mwandishi: Wakio Mbogho, DW, Nakuru
Mhariri: Daniel Gakuba