Baraza la Seneti DRC kujadili hatma ya Kabila
23 Mei 2025Baraza la seneti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, litajadili leo kuhusu suala la kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa rais wa zamani wa nchi hiyo Joseph Kabila,ambaye anatuhumiwa na serikali, kuliunga mkono kundi la waasi laM23 mashariki mwa nchi hiyo.
Serikali ya kinshasa, inamshutumu Kabila kwa uhaini, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu pamoja na kushirikiana na kundi linaloendesha uasi.
Waziri wa sheria Constant Mutamba mwezi uliopita alizitolea mwito mahakama za kijeshi nchini humo kuifuatilia kesi hiyo dhidi ya Kabila ambaye aliiongoza Kongo kati ya mwaka 2001 na 2019.
Ili kufungua njia ya kuanzishwa mchakato wa kisheria dhidi ya kiongozi huyo wa zamani, mwendesha mashtaka ya umma wa jeshi la Kongo alipeleka ombi kwenye baraza la Seneti kumvua, kinga ya kutoshtakiwa.