Baraza la Israel kuidhinisha ukaliaji kamili wa Gaza
5 Agosti 2025Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Israel, mpango huo unahusisha uvamizi kamili wa Ukanda wa Gaza na kurejesha udhibiti wa eneo hilo.
Ingawa bado haijathibitishwa rasmi, vyombo vya habari vinaripoti kuwa Netanyahu amekwishatoa maagizo ya kupanua mashambulizi hadi maeneo ambako mateka wanashukiwa kushikiliwa.
Vita hivyo, ambavyo sasa vinaingia mwezi wa 22 tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 yaliyofanywa na Hamas na kusababisha vifo vya zaidi ya Waisraeli 1,200 na utekaji wa watu 251, vimesababisha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, watu zaidi ya 60,933 wameuawa, huku mashirika ya kibinadamu yakionya kuwa wakaazi wa Gaza wapatao milioni 2.4 wanakabiliwa na baa la njaa la kiwango cha kutisha.
Upinzani ndani na nje ya Israel
Hata hivyo, mpango wa Netanyahu wa kuongeza mashambulizi unakumbwa na upinzani mkubwa, si tu kutoka kwa Wapalestina na jumuiya ya kimataifa, bali pia kutoka ndani ya Israel.
Nchini Israel, familia za mateka waliobaki zimekuwa zikiishinikiza serikali kusitisha mapigano ili kufanikisha kuachiliwa kwa wapendwa wao.
Kundi la mamia ya maafisa wa zamani wa usalama nchini humo pia limetia saini barua ya wazi likitaka vita vikomeshwe, likieleza kuwa Hamas haileti tena tishio la kimkakati kwa Israel.
Akizungumza na DW, aliyekuwa balozi wa Israel nchini Ujerumani, Jeremy Issacharoff, alisema:
"Ni muhimu sana tufanye kila juhudi ndani ya mfumo wa ulinzi wa Israel kuwaokoa mateka 50 waliobaki Gaza. Tunakadiria kuwa takriban watu 20 bado wako hai, na waliobaki wanahofiwa kuwa wamekufa. Hii ni fursa muhimu ya kumaliza vita na kufunga ukurasa huu wa huzuni uliotikisa sana jamii ya Kiyahudi."
Wakati huo huo, Hamas imesema iko tayari kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu kupeleka misaada kwa mateka ikiwa Israel itafungua njia za kibinadamu kwa kudumu na kusitisha mashambulizi wakati wa usambazaji wa misaada.
Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas, Husam Badran, aliiambia Al Jazeera kuwa "mpira sasa uko mikononi mwa Israel na Marekani," akidai kuwa wao ndio wanaochelewesha makubaliano ya kusitisha mapigano.
Nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, alikutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisaidiwa na washirika wa Marekani ili kuelekeza mjadala zaidi kwa suala la mateka, badala ya njaa inayoshuhudiwa Gaza.
Shinikizo la kimataifa, mzozo wa kisiasa wa ndani
Katika kukabiliana na shinikizo la kimataifa kuhusu hali ya kibinadamu, idara ya kiraia ya wizara ya ulinzi ya Israel, COGAT, imetangaza mpango wa kuruhusu biashara za binafsi katika Ukanda wa Gaza chini ya uangalizi mkali.
Kwa mujibu wa COGAT, wafanyabiashara wachache waliokidhi vigezo vya kiusalama wameidhinishwa kupeleka bidhaa muhimu kama chakula, maziwa ya watoto na vifaa vya usafi.
Mchakato huo mpya unalenga kupunguza utegemezi wa Gaza kwa misaada ya UN na misafara ya kimataifa, huku bidhaa zikiwa zinapitishwa kwenye ukaguzi mkali wa kijeshi ili kuzuia kuifaidisha Hamas.
Wakati mzozo huu wa kivita ukiendelea, hali ya kisiasa ndani ya Israel imezidi kugubikwa na migogoro. Jumatatu, Baraza la Mawaziri lilipiga kura ya kumfuta kazi Mwanasheria Mkuu, Gali Baharav-Miara, hatua iliyochochea mvutano zaidi kati ya Netanyahu na taasisi ya mahakama.
Mahakama ya Juu imeisimamisha hatua hiyo kwa muda huku ikitathmini uhalali wake. Wakosoaji wanasema hatua hiyo inalenga kuingilia uhuru wa mahakama, hasa ikizingatiwa kuwa Netanyahu anakabiliwa na kesi za ufisadi.
Juhudi za awali za serikali kubadili mfumo wa mahakama mwaka 2023 zilisababisha maandamano makubwa ya umma.