Baraza la Haki za binadamu la UN kuijadili DRC
4 Februari 2025Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linajiandaa kufanya kikao cha dharura siku ya Ijumaa, kuujadili mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Msemaji wa baraza hilo Paschal Sim amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba kikao hicho kimeitishwa kufuatia ombi la serikali ya Kongo lililotolewa jana Jumatatu.
Baraza hilo kimsingi ndio chombo cha juu zaidi katika Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya haki za binadamu na kwa hakika kilikuwa hakina ratiba ya kukutana hadi mwishoni mwa Februari.Soma pia: M23 yaendelea kuchukua udhibiti wa maeneo mashariki mwa Kongo
Lakini ombi la serikali ya mjini Kinshasa kufuatia hali inayoendelea mashariki mwa nchi yake, kumelifanya baraza hilo lenye jumla ya wanachama 47, Kongo ikiwa ni miongoni mwa wanachama hao, kuitisha mkutano huo wa dharura.
Waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda wiki iliyopita waliuteka mji wa Goma huko Kivu Kaskazini eneo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa Kongo na kusababisha umwagaji damu kwenye eneo hilo.
Wasiwasi wa kutekwa mji wa Bukavu
Japokuwa mapigano yamesitishwa katika mji huo wenye wakaazi zaidi ya milioni moja bado machafuko yameenea katika mkoa jirani wa Kivu Kusini na kusababisha khofu kubwa kwamba kundi hilo la waasi linasonga mbele kuelekea mji wa Bukavu.
Fazili Mubole, afisa wa shirika moja la kiraia amezungumzia wasiwasi walionao kwa kusema hivi.
"Taarifa iliyotolewa na M23 ya kusitisha vita inaonesha bado huu ni mkakati wao wa kijeshi. Na wakati huo huo, wanaposema kwamba mji wa Bukavu haupaswi kuchukuliwa, huo ni mkakati wao wa kujiimarisha, na kujipanga upya kwa wapiganaji na silaha na hapo hapo wakisonga mbele kuelekea kuuchukuwa mji wa Bukavu. Na ndio sababu bado tunaziomba mamlaka kutoiamini taarifa kama hii na inatakiwa mamlaka iwe tayari kuwamaliza maadui wa jamhuri.''
Jumatatu M23 ilitangaza itasitisha vita leo Jumanne kwa lengo la kupisha shughuli za kibinadamu kuanzia, na tangazo hilo limetolewa siku kadhaa kabla ya mkutano wa dharura uliopangwa kufanyika kati ya Rais Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC, kwa mujibu wa Kenya ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Uganda yatuma kikosi cha ziada DRC
Uganda nayo wiki iliyopita ilipeleka zaidi ya wanajeshi 1,000 wa ziada huko mashariki mwa Kongo karibu na eneo ambako Kinshasa inapambana na waasi wa M23. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vinne vya kidiplomasia na Umoja wa Mataifa. Hatua hiyo imezidisha wasiwasi, mgogoro huo huenda ukatanuka kwenye kanda nzima.Soma pia: HRW yasema mzozo wa nchini Kongo unaweza kuwa 'janga'
Huku hayo yakiripotiwa, mamia ya Wakongomani walijitokeza hii leo kuandamana mbele ya ofisi za Umoja wa Ulaya nchini Afrika Kusini kudai Rwanda iwekewe vikwazo, kutokana na hatua yake ya kuwaunga mkono waasi wa M23.
Takriban waandamanaji 2,000 wakiwa na mavazi ya rangi za bendera ya nchi yao Kongo, buluu, njano na nyekundu walisikika wakiimba nje ya ubalozi wa Umoja wa Ulaya katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, huku wakishikilia mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kutaka Kongo iwe huru na kuutambuwa mchango kikosi cha jeshi la Afrika Kusini na jeshi la nchi yao, wanaojaribu kulikomboa eneo la mashariki.
Waandamanaji walisikika wakiutaka Umoja wa Ulaya kupitisha vikwazo dhidi ya Rwanda kama walivyofanya dhidi ya Urusi kufuatia vita vyake nchini Ukraine.
Waandamanaji hao raia wa Kongo pia wamelaani mpango wa biashara ya madini kati ya Umoja wa Ulaya na Rwanda wakiituhumu Brussels kwamba inachochea vita mashariki mwa Kongo huku ikipora mali ya taifa lao hilo.