Baraza Kuu la Bunge lakutana Afghanistan
14 Desemba 2003Matangazo
KABUL: Mfalme wa zamani wa Afghanistan Mohammed Sahir Shah ameufungua mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Bunge mjini Kabul. Wajumbe 500 wa Baraza hilo liitwalo LOYA JIRGA wanaotokea kila sehemu ya nchi, wamekuja katika mji mkuu kushauriana juu ya mswada wa katiba mpya juu ya kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Afghanistan. Katika hutuba yake ya mafunguzi, Rais Hamid Karsai aliwaita wajumbe wa mkutano huo waikubali katiba hiyo mwishoni mwa mkutano wa Baraza Kuu. Hatua hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa Afghanistan, alisema Rais Karsai. Mkutano wa LOYA JIRGA unatazamiwa kuweka msingi wa kuanzishwa utawala wa kidemokrasi nchini Afghanistan baada ya kuangushwa utawala wa Taliban. Juhudi hizo za kidemokrasi zilianzishwa hapa Ujerumani katika Mkutano wa Petersburg, karibu ya Bonn, miaka miwili iliyopita.