Bangladesh: Hatuwezi tena kuwasaidia wakimbizi wa Rohingya
25 Agosti 2025Muhammad Yunus ameiomba jamii ya kimataifa kusaka suluhu endelevu kuelekea mzozo huo wa wakimbizi.
Ametoa matamshi hayo kwenye maadhimisho ya miaka minane tangu zaidi ya wakimbizi 700,000 walipoingia kwenye mji wa pwani ya Bangladesh wa Cox's Bazar, na kuugeuza kuwa makazi makubwa zaidi ya wakimbizi ulimwenguni.
Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobeli amesema wakimbizi wameielemea Bangladesh, kuanzia kiuchumi, mazingira hadi kiutawala na kuiomba jumuiya ya kimataifa kuandaa mpango unaoweza kutekelezwa, kuwawezesha wakimbizi hao kurejea nyumbani.
Wakimbizi wengine 150,000 wameingia Bangladesh kutokea jimbo la Rakhine, mashariki mwa Myanmar kufuatia mapigano makali kati ya vikosi vya serikali ya kijeshi na Jeshi la Arakan, lenye idadi kubwa ya wapiganaji wa madhehebu ya Buddha.