Balozi za Magharibi zahimiza amani Kenya
24 Juni 2025Matangazo
Mabalozi wa nchi za Magharibi nchini Kenya wametoa wito wa kuwepo kwa uvumilivu na utulivu, wakati taifa hilo likijiandaa kwa maandamano ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya umwagaji damu mwaka jana.
Mabalozi hao wamesema wana wasiwasi kufuatia taarifa za madai ya vikundi vya wahuni kulipwa ili kuvuruga maandamano.
Hali ya taharuki imeongezeka baada ya waandamanaji waliopinga ukatili wa polisi wiki iliyopita kukabiliwa na watu wenye silaha wanaodaiwa kushirikiana na polisi.
Mashirika ya haki za binadamu yameripoti vifo vya takriban watu 60 kati ya Juni na Julai mwaka jana.
Katika tamko la pamoja, mabalozi kutoka Ujerumani, Uingereza, Marekani, Canada na mataifa mengine wametoa wito kwa maandamano ya kesho kufanyika kwa amani.