Balozi wa zamani Ukraine atoa ushahidi kesi ya Trump
16 Novemba 2019Balozi wa zamani wa Marekani nchini Ukraine Marie Yovanovitch ametoa ushahidi kuhusu kuondolewa kwake ghafla katika wadhifa wake wakati wa siku ya pili ya kusikilizwa hadharani ushahidi unaoweza kupelekea kufunguliwa mashtaka na kuondolewa madarakani kwa Rais Donald Trump.
Wakati wa ushahidi wake mbele ya Kamati ya Bunge ya Ujasusi, Trump alikuwa kwenye mtandao wa Twitter akimshambulia mwanadiplomasia huyo na rekodi yake.
Aliandika kuwa kila mahali alikofanya kazi Marie Yovanovitch mambo yalikwenda mrama. Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge Mdemocrat Adam Schiff aliisoma kauli hiyo ya Trump kwa Yovanovitch wakati wa kikao hicho, akimuuliza jibu lake.
"Siwezi kuzungumzia kile rais anajaribu kukifanya, lakini nadhani athari ni kutisha," alisema. Ujumbe huo wa Twitter ulizusha shutuma za haraka, huku Wademocrat wakisema kilikuwa kitendo cha kuwatisha mashahidi.
Yovanovitch anayefahamika kwa rekodi yake ya kupambana na rushwa, alipelekwa Ukraine 2016 ambako alihudumu kama balozi wa Marekani hadi alipolazimika kuondoka Mei 2019.
Schiff alisema kuondolewa kwake kulisaidia kuweka mazingira ya kufunguliwa njia isiyo rasmi, ya kuendesha sera ya Ukraine ambayo ilitumiwa na Trump na washirika wake kuishinikiza Ukraine kuwachunguza wapinzani wa kisiasa wa rais huyo.
Yovanovitch anaungana na maafisa wengine kutoa ushahidi kwenye mchakato wa kihistoria ambao wanachama wa Democratic wanautegemea kupata hoja za kumfungulia mashtaka yanaweza kumuondoa madarakani rais Trump.