BAGHDAD:Wanawake na watoto kuanza kupekuliwa nchini Iraq.
28 Septemba 2005Mkuu wa jeshi la polisi nchini Iraq,amesema leo kuwa kuanzia sasa wanawake na watoto watapekuliwa katika vituo vya ukaguzi kama vile wanavyofanyiwa wanaume,baada ya vijana sita waliokuwa katika msururu wa kujiandikisha kujiunga na jeshi kuuawa na wengine 30 kujeruhiwa,katika mji wa kaskazini wa Tal Afar,wakati wa shambulio la kwanza kufahamika,lililomhusisha mripuaji wa kujitoa muhanga mwanamke.
Kwa mujibu wa Jenerali Ahmed Mohammed Khalaf,shambulio la leo linaonekana ni mwanzo wa mbinu mpya,zinazotazamiwa kutumiwa na wanamgambo wanaoendesha harakati zao nchini Iraq,kwa kuwatumia wanawake ambao ni mara chache kupekuliwa katika vituo vya ukaguzi vya Tal Afar,kwa vile taratibu za kidini na utamaduni wa kijamii haukubaliani na upekuzi kwa wanawake.
Mwanamke huyo aliyejizonga mabomu,alijiripua nje ya kambi ya jeshi inayoandikisha wanajeshi wapya leo mchana,katikati ya mji wa Tal Afar,kilometa 150 mashariki na mpaka wa Syria.