BAGHDAD:Wanamgambo wa Iraq wajipenyeza ndani ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
21 Septemba 2005Watawala nchini Iraq wamekiri kuwa vikundi vya wanamgambo vinavyoipinga serikali,wamemudu kujipenyeza ndani ya vikosi vya usalama vya taifa na hatimaye kudhoofisha utendaji kazi wa vyombo hivyo.
Hayo yameelezwa baada ya jeshi la Uingereza kueleza kuwa liliwajibika kutumia nguvu kuingia katika gereza la mjini Basra kufanikisha kuachiliwa huru wanajeshi wake wawili,baada ya kubaini kuwa askari hao waliokuwa wanashikiliwa,walikabidhiwa kwa kikundi kimoja cha wanamgambo.Baadae wanajeshi hao wawili walikutwa katika nyumba moja jirani na gereza hilo.
Tukio hilo baadae liliibua machafuko makubwa kati ya vikosi vya jeshi la Uingereza na raia wa mji wa Basra.
Wanajeshi hao wawili wa Uingereza waliodhaniwa wakifanya kazi za kijasusi,walitiwa mbaroni na polisi wa Iraq juzi siku ya Jumatatu baada ya kutuhumiwa kuwafyatulia risasi polisi hao.