BAGHDAD:Umwagikaji damu Iraq waendelea
11 Agosti 2005Jeshi la Marekani nchini Iraq limearifu wanajeshi sita wa Marekani wameuwawa katika mashambulizi yaliyofanywa sehemu mbali mbali za Iraq.
Wanajeshi wanne wa Marekani waliuwawa na wengine sita wakajeruhiwa kwenye shambulio lililofanywa karibu na mji wa Baiji.
Mwanajeshi mmoja wa Marekani aliuwawa kwenye shambulio la bomu la kujitoa muhanga la ndani ya gari mjini Baghdad huku mwanajeshi wa sita akiuwawa kwa kupigwa risasi wakati wa mapambano ya kijeshi karibu na mji wa Habbaniyah kaskazini ya Iraq.
Wakati huo huo viongozi wa ngazi ya juu wa Iraq wamefanya mazungumzo ya kutatua mzozo juu ya suala la katiba mpya.
Katiba hiyo inatarajiwa kufikishwa bungeni ifikiapo Agosti 15.
Hii leo makundi ya viongozi wa madhehebu ya wasunni,washia pamoja na wakurdi wanatarajiwa kukutana.
Masuala nyeti yanayoichelewesha katiba mpya ni pamoja na jukumu la dini ya kiislamu na haja ya kuwepo serikali ya shirikisho.