BAGHDAD.Mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga yazidi Iraq
15 Juni 2005Takriban watu 20 wameuwawa na wengine 60 wamejeruhiwa katika mkasa wa bomu la kujitoa muhanga katikati ya soko katika mji wa Kirkuk ulio kilomita 250 kaskazini mwa Iraq.
Katika shambulizi jingine la bomu la kujitoa muhanga wanajeshi watano wa Iraq wameuwawa baada mshambulizi wa kujitoa muhanga kujilipua karibu na mji wa Baquba kaskazini mwa Baghdad.
Wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld amekiri kuwa hali ya usalama si thabiti nchini Iraq tangu kung’olewa mamlakani Saddam Hussein miaka miwili iliyopita.
Lakini bwana Rumsfeld hakuchelea kuzilaumu nchi jirani za Iran na Syria kuwa ndio zinachangia hali hiyo kwani zinawaruhusu wapiganaji wenye msimamo mkali kuvuka na kuingia nchini Iraq kupitia mipaka yao.
Kwingineko waziri huyo wa ulinzi wa Marekani ametetea kuendelea kuwepo jela ya Guantanamo Bay licha ya shinikizo kutoka kwa wanasiasa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu za kuitaka Marekani iifunge jela hiyo.