BAGHDAD:Mashambulio ya Mabomu yaendelea kushuhudiwa Iraq
31 Julai 2005Raia wawili wa Uingereza wanaofanyia kazi kampuni ya kibinafsi ya usalama nchini Iraq yenye makao yake Uingereza wameuwawa kwenye mambulio ya bomu la kutegwa kando mwa barabara.
Kwa mujibu wa msemaji kutoka ubalozi mdogo wa Uingereza msafara wa magari ya waingereza hao ulishambuliwa wakati ulipokuwa unapitia barabara ya eneo la kusini magharibi ya mji wa Basra.
Katika tukio jingine mjini Baghdad hii leo bomu la kutegwa ndani ya gari katika kituo cha ukaguzi wa polisi kusini ya Baghadad liliripuliwa kwa kutumia rimoti na kuwauwa watu watano na kuwajeruhi wengine kumi.
Kwa mujibu wa Polisi shambulio hilo limefanyika kilomita hamsini kusini ya baghdad karibu na mji wa Haswa.
Gari lililokuwa limejazwa mabomu liliegeshwa karibu na barabara karibu na kituo hicho na kisha kuripuliwa kwa rimoti.
Habari zaidi kutoka nchini humo zimearifu afisa wa ngazi ya juu kutoka wizara ya afya ametekwa nyara.Imane Naji Abdelrazaak alitekwa nyara kwa mtutu wa bunduki kutoka nyumbani kwake.
Taarifa zaidi kuhusu utekaji nyara huo hazijatolewa.