BAGHDAD:Kiongozi namba 2 wa Alqaeda nchini Iraq auwawa
28 Septemba 2005Katika tukio la umwagikaji wa damu watu kiasi cha kumi wameuwawa na zaidi ya wengine 25 wamejeruhiwa kwenye shambulio la bomu la kutegwa ndani ya gari lililotokea mjini Baghdad karibu na kituo cha kuwaandikisha polisi.
Wakati huo huo polisi kwenye mji wa Kut wamezipata maiti za watu 22 waliouwawa kwa kupigwa risasi wakiwa wamefungwa.
Kwengineko nchini humo wanajeshi wa Marekani wamearifu kwamba wamemuua kwa kumpiga risasi kiongozi wa pili wa kundi la Al Qaeda.
Abu Azzam aliuwawa mjini Baghdad siku ya jumatatu wakati wa uvamizi uliofanywa kwa pamoja na wanajeshi wa Marekani na wa Iraq.
Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Marekani Azzam alipatikana akiwa amejificha kwenye jumba moja baada ya kutonywa habari na mkaazi mmoja.
Kiongozi huyo wa Alqaeda anaaminika kuwa nyuma ya mashambulio mengi mjini Baghdad ambayo yamesababisha mauwaji ya watu kiasi cha 1200.
Azzam ni kiongozi wa pili wa Aqaeda nchini Iraq baada ya Musab Alzarqawi ambaye bado anawindwa na wanajeshi.