BAGHDAD:Helikopta ya Marekani yadenguliwa Baquba Iraq
27 Mei 2005Helikopta ya kijeshi ya Marekani imeanguka baada ya kudenguliwa karibu na mji wa Baquba kaskazini mwa Baghdad.Kamanda wa jeshi la Marekani amesema hatma ya watu wawili walikuwemo ndani ya ndege hiyo hajajulikana.Helikopta nyingine hata hivyo ya Marekani imefanikiwa kutuwa salama.
Tukio hilo limetokea baada ya waziri wa ulinzi wa Iraq Sadoun Al Dulaimi kutangaza operesheni kabambe dhidi ya waasi mjini Baghdad.
Operesheni hiyo dhidi ya waasi itavijumuisha pamoja zaidi ya vikosi vya wanajeshi elfu 40 kutoka wizara za ulinzi na usalama wa ndani nchini humo.
Operesheni hiyo itakuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa na vikosi vya usalama vya Iraq mjini Baghdad.
Wakati huo huo kumekuwa na taarifa za kutatanisha kutoka kwa viongozi wa Iraq juu ya kujeruhiwa kwa kiongozi wa mtandao wa Alqaeda nchini humo Abu Musab Al Zaqawi.
Waziri wa ndani Bayan Jabor amesema amepokea habari hiyo lakini waziri mkuu Ibrahim Aljafari amesema hakuna taarifa kama hiyo iliyothibitishwa.
Wapiganaji wametuma taarifa katika mtandao wa Internet kwamba Zarqawi anauguza jeraha la risasi kwenye mbavu.
Katika tukio jingine waasi wamempiga risasi na kumuua afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya viwanda na madini mjini Baghdad.