BAGHDAD-Waziri Mkuu mpya wa Iraq kuteuliwa leo.
7 Aprili 2005Baraza jipya la Urais nchini Iraq,leo linatazamiwa kumteua Waziri Mkuu mpya kutoka madhehebu ya Shia,baada ya kumteua kiongozi wa Kikurdi Jalal Talabani,kuwa rais.
Wabunge wanatabiri kuwa ni lazima serikali mpya itakuwa imeanza kazi wiki ijayo,ikiwa na Waziri Mkuu anayepewa nafasi ya kushika hatamu,ambaye ni Mshia,Ibrahim al-Jaafari,hivyo kutoa nafasi kwa serikali hiyo kuanza kazi baada ya zaidi ya miezi miwili tangu ulipofanyika uchaguzi wa kihistoria nchini Iraq.
Kuteuliwa kwa Bwana Jaafari,kiongozi wa chama cha Dawa,kutakuwa ni enzi mpya ya Jumuia ya Washia walio wengi kushika hatamu ya uongozi katika serikali ya Iraq baada ya miongo kadhaa ya kukandamizwa.
Kazi nyingine inayokusudiwa kutekelezwa na Bunge la Iraq pamoja na serikali mpya,ni kupitia mapendekezo ya katiba mpya na kuweka mazingira yatakayowezesha kufanyika uchaguzi mkuu mpya mwezi wa Disemba mwaka huu.
Akiapishwa kushika hatamu ya uongozi wa Iraq,rais mpya wa nchi hiyo Bwana Talabani,aliahidi kufanya kila awezalo kuviunganisha vikundi vinavyohasimiana na kuifanya Iraq iwe nchi moja.