Baghdad. Watu 24 nchini Iraq wauwawa kwa bomu la kujitoa muhanga.
13 Julai 2005Raia 24 nchini Iraq , wengi wao wakiwa watoto, wameuwawa kutokana na bomu la kujitoa mhanga katika gari lililokuwa limelengwa dhidi ya wanajeshi wa Marekani.
Kiasi cha watoto 20 zaidi wamejeruhiwa katika mlipuko huo, ambao pia umesababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Marekani na wengine watatu wamejeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea wakati wanajeshi wa Marekani walikuwa wakiwapa watoto peremende, baada ya kuingia katika eneo lao mjini Baghdad wakitoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea shambulio.
Wakati huo huo afisa mwandamizi katika wizara ya mambo ya ndani nchini Iraq amekiri kuwa watu kumi wamekufa kwa kukosa hewa katika gari ya polisi baada ya kukamatwa. Amesema kuwa wale waliohusika watafikishwa mahakamani. Tukio hilo limewakasirisha Wairaq wengi wakati hali ya wasi wasi kati ya Wasunni na serikali inayomilikiwa na Washia ikizidi kupanda.