Baghdad. Wanajeshi 15 wauwawa na magaidi nchini Iraq.
9 Aprili 2005Nchini Iraq, wapiganaji wa chini kwa chini wamewapiga risasi na kuwauwa wanajeshi 15. Polisi wa Iraq wamesema kuwa shambulio hilo lilitokea jana Ijumaa karibu na mji wa Latifia, ambao uko kilometa 50 kusini magharibi ya mji mkuu Baghdad. Wamesema pia pia kuwa wanajeshi hao wa Iraq walikuwa wanasafiri katika lori, ambalo lilisimamishwa na watu hao wenye silaha na baadaye kuwapiga risasi.
Wakati huo huo mamia kwa maelfu ya wananchi wa Iraq wa madhehebu ya Shia walikusanyika katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad wakiandamana kuipinga Marekani , wakiadhimisha miaka miwili tangu mji huo kuchukuliwa na majeshi ya Marekani. Na kama uthibitisho wa kuwako hali ya wasi wasi nchini Iraq, msaidizi wa kiongozi wa madhehebu ya Shia mwenye siasa kali za kuipinga Marekani , Moqtada Sadr ameuwawa mjini Baghdad wakati akiwa njiani kuhudhuria maandamano hayo.