Baghdad. Wajumbe wa kutunga katiba nchini Iraq kutoka katika kundi la Wasunni waamua kurejea katika kamati hiyo baada ya mgomo.
25 Julai 2005Wajumbe wa kamati ya kutunga katiba mpya ya Iraq , Waarabu wa madhehebu ya Sunni wamesema kuwa watamaliza mgomo wao na kurejea katika kamati hiyo.
Wasunni hao waliondoka katika majadiliano baada ya mmoja wa wajumbe wao kuuwawa wiki iliyopita.
Wamekubaliana kujiunga tena na mazungumzo hayo baada ya bunge la Iraq kusema kuwa litakubali madai yao yote.
Kundi hilo la Wasunni lilitaka kupewa ulinzi zaidi na uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na mauaji hayo.
Waarabu wa madhehebu ya Sunni, ambao walikuwa ndio wenye madaraka wakati wa utawala wa Saddam Hussein , ni asilimia 20 ya idadi ya wakaazi wa Iraq.
Kuhusika kwao katika uandikaji wa katiba unaonekana kuwa ni muhimu kwa ajili ya uthabiti wa hali ya kisiasa katika nchi hiyo.
Muswada huo wa katiba ni lazima uidhinishwe na bunge hapo August 15.