Baghdad: Utekaji nyara unaendelea huko Iraq
6 Julai 2005Kikundi cha gaidi wa kutokea Jordan, Abu Mussab al-Sarkawi, kimekiri kwamba ndicho kilichomteka nyara balozi wa Misri katika Iraq. Balozi al-Shariff alitekwa nyara mwisho wa wiki iliopita huko Baghdad. Haijulikani watekaji nyara wametoa madai gani. Jana balozi wa Pakistan huko Baghdad, Yunus Khan, alikosewa chupu chupu kuuliwa. Hapo kabla makamo wa balozi wa Bahrein katika Iraq alinusurika chupu chupu na kutekwa nyara. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, amefadhaishwa na vitendo hivyo. Yeye anahofia kwamba utayarifu wa jamii ya kimataifa kuisaidia Iraq katika wakati huu muhimu unaweza ukapata pigo kutokana na visa hivyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Kiarabu, Arab League, Amr Musa, alisema huko Kairo kwamba lengo la watekaji nyara ni kuuharibu uhusiano baina ya Iraq na nchi za Kiarabu.