Baghdad. Serikali ya Iraq huenda ikatajwa baada ya saa 24.
26 Aprili 2005Kundi kubwa la kisiasa nchini Iraq limesema leo kuwa linaongeza kasi ya mazungumzo ya muungano katika juhudi za kupata makubaliano ya kuundwa kwa serikali mpya katika muda wa saa 24 zijazo huku jumuiya ya kimataifa ikitoa shinikizo kali, karibu miezi mitatu baada ya kufanyika nchini humo uchaguzi wa kihistoria.
Msemaji wa muungano wa vyama vya kisiasa vya Washia vya United Iraq Alliance Jawad Talib ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ifikapo kesho Jumatano serikali itakuwa imetangazwa.
Jawad al Maliki makamu mwenyekiti wa chama cha Dawa cha waziri mkuu mteule Ibrahim al-Jaafari amesema kuwa baraza jipya la mawaziri linatarajiwa kuwajumuisha pia manaibu waziri mkuu watatu.
Wasaidizi wa Bwana Ahmed Chalabi ambaye alikuwa akiungwa mkono na wizara ya ulinzi ya Marekani hapo kabla na ambaye alishinda katika uchaguzi kupitia muungano wa Washia, wamesema kuwa huenda atakuwa mmoja kati ya manaibu waziri mkuu, akihusika na wizara muhimu ya mambo ya ndani na ulinzi.
Waendesha majadiliano wamesema kuwa wameacha sasa juhudi zao za kuwashawishi wanaomuunga mkono waziri mkuu anayeondoka madarakani Iyad Allawi kujiunga na serikali hiyo.