BAGHDAD : Rice ziarani Iraq kuangalia hali ya usalama na uchumi
15 Mei 2005Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice amefanya ziara ya ghafla nchini Iraq leo hii na kuitaka serikali changa ya nchi hiyo kuwajumuisha wajumbe wapya wa madhehebu ya Sunni katika kazi ngumu ya kurasimu katiba mpya.
Rice akiwa katika ziara yake ya kwanza nchini Iraq tokea ashike wadhifa huo mkuu wa kidiplomasia wa Marekani ameingia nchini humo kwa siri chini ya ulinzi mkali kwa kutumia ndege ya kijeshi AC-17 kuonyesha uungaji mkono wa Marekani kwa serikali ya nchi hiyo inayojaribu kudhibiti mfarakano wa kikabila huku ikipambana na uasi unaopamba moto.
Rice kwanza alitua katika mji wa kaskazini wa Wakurdi wa Arbil na baadae kwenda kwa kutumia helikopta katika mji ulio karibu wa Salahuddin kukutana na kiongozi wa Wakurdi Massoud Barzani kabla ya kwenda Baghdad kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Ibrahim Jaafari,Rais Jamal Talabani pamoja na maafisa wengine wa serikali.
Rice ameelezea wasi wasi wake juu uwakilishi wa Wasunni kwenye kamati iliyochaguliwa na bunge wiki iliopita kurasimu katiba ambayo imehodhiwa na Washia na Wakurdi ikiwa na Wasunni wawili tu miongoni mwa wajumbe wake 55.
Rice pia amesema anataka kuangalia hali ya usalama na nyanja uchumi nchini humo.