Baghdad. Operesheni radi yawanasa wapiganaji 700 nchini Iraq.
4 Juni 2005Viongozi wa Iraq wamewakamata wapiganaji wa chini kwa chini zaidi ya 700 na kuwauwa wengine 28 katika siku tano za mwanzo za operesheni iliyopewa jina la Radi. Msako huo ulitangazwa katika juhudi za kusimamisha mashambulizi ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 12,000 katika muda wa miezi 18 iliyopita.
Siku ya Alhamis pekee , kiasi cha watu 50 wameuwawa nchini Iraq katika matukio tofauti manne ya mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga ama mashambulio mengine.
Katika shambulio moja kubwa , mtu mmoja amejilipua katika mkusanyiko wa Waislamu wa madhehebu ya Sufi kaskazini ya Baghdad, na kuuwa watu kumi. Hili ni tukio la kwanza kubwa la mashambulizi dhidi ya jamii hiyo ndogo ya Waislamu wa madhehebu ya Sufi nchini Iraq.