Baghdad. Operesheni Matador yakamilika nchini Iraq, lakini bado wapiganaji wa chini kwa chini waendelea kushambulia.
15 Mei 2005Jeshi la Marekani limesema limewauwa wapiganaji wa chini kwa chini 125 katika shambulio magharibi ya Iraq ambalo limemalizika jana Jumamosi lakini wapiganaji hao wameshambulia tena mjini Baghdad, wakimuua afisa wa ngazi ya juu wa serikali pamoja na kushambulia polisi wa doria.
Operasheni hiyo iliyochukua muda wa wiki nzima ililengwa katika kuwafukuza wapiganaji hao kutoka katika ngome yao katika jimbo la Anbar, eneo ambalo lina wapiganaji wengi wa chini kwa chini.
Taarifa ya jeshi la Marekani imesema kuwa katika operesheni hiyo , jeshi hilo lilifanikiwa kudhoofisha upinzani wa wapiganaji hao katika eneo hilo na kuwauwa wapiganaji 125, wakiwajeruhi wengi wengine, na kuwakamata wapiganaji 39 ambao wanaumuhimu mkubwa katika kupata taarifa za kiusalama. Jeshi hilo limesema wanajeshi wao 9 wameuwawa na wengine 40 kujeruhiwa katika operesheni hiyo iliyokuwa na lengo la kuvunja ngome za wapiganaji ambazo zimekuwa zikitumika kupanga mashambulizi dhidi ya miji ya Falluja, Ramadi, Mosul na Baghdad.
Wakati huo huo gazeti moja la Uingereza limesema, Abu Musab al- Zarqawi, mtu anayetafutwa sana na majeshi ya Marekani nchini Iraq, amejeruhiwa na kupatiwa matibabu kwa muda katika hospitali nchini humo wiki iliyopita kabla ya kutoweka na watu wake.