BAGHDAD: Mwenyekiti wa baraza tawala la Iraq amesema kwamba ...
27 Novemba 2003Matangazo
kiongozi wa cheo cha juu wa madhehbu ya Shia anataka ufanywe uchaguzi kamili katika nchi hiyo. Kiongozi huyo wa Kishia, Ayatollah Sistani, alikutana na baraza la utawala kuzungumzia wasiwasi waliokuwa nao mashehe wa madhehbu ya Shia kuhusu mipango ya Marekani ya kukabidhi madaraka kwa Wa-Iraqi. Mwenyekiti wa baraza hilo, Jalal Talibani, alisema Ayatollah Sistani anaipinga mipango hiyo kwa vile inataka iweko taasisi ambayo haitachaguliwa moja kwa moja na umma na ambayo itateuwa serekali ya mpito na kusimamia kuandikwa katiba mpya.
Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, Jack Straw, alisema hapo awali huko Baghdad kwamba majeshi ya Muungano yatasonga mbele kuleta utulivu katika Iraq. Bwana Straw alikiri kwamba Muungano unaoongozwa na Marekani bado utabidi upambane na upinzani katika nchi hiyo na mashambulio yanayofanywa dhidi ya majeshi ya Muungano hayajazistaajabisha Uengereza wala Marekani..
Na waziri wa ulinzi wa Marekani, Donald Rumsfeld, amesema vikosi vitatu zaidi vya wanajeshi wa nchi kavu alfu tatu wa Kimarekani vitapelekwa Iraq.
Pia kombora lililipiga jana jengo la ubalozi wa Italy mjini Baghdad. Jengo hilo liliharibiwa, lakini hakuna mtu aliyeumia. Mwanzoni mwa mwaka huu shambulio la kujitolea mhanga liliwauwa wanajeshi 19 wa Kitaliana katika mji wa kusini wa Nassiriya. Tangu wakati huo majeshi ya Kitaliana katika Iraq yamewekwa katika hali ya tahadhari. Pia jeshi la Marekani limesema askari wake 2,000 wamefanya msako mkubwa katika eneo lililoko nje kidogo ya Baghdad. Hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kupambana na upinzani.
Matangazo